
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema takribani watu laki mbili nchini wana ugonjwa wa Selimundu (Sickle Cell), na watoto 11,000 huzaliwa wakiwa na ugonjwa wa Selimundu unaohusisha kurithi vinasaba toka kwa wazazi ndani ya mwaka mmoja, huku tafiti zikionyesha kuwa sehemu zenye maambukizi ya ugonjwa wa malaria kwa wingi ndizo ambazo zina wagonjwa wengi wa ugonjwa huo.
.
Dkt.Mollel ameyasema hayo Bungeni Jijini Dodoma, wakati akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu, lililoulizwa na Mbunge wa Viti Malum, Mhe. Fatma Hassan Toufiq, aliyeuliza ni Watanzania wangapi wenye tatizo la Selimundu na ni Mikoa mingapi imeathiriwa na ugonjwa huo.
.
Aidha, Dkt. Mollel, amesema kwa mujibu wa takwimu za Mfumo wa Taarifa za Uendeshaji wa Huduma za Afya (MTUHA) zinaonesha kuwa jumla ya wagonjwa Elfu 86,990 wa Sickle Cell walihudumiwa kwa mwaka 2022, ambapo ametoa wito kwa wananchi wanaotarajia kufunga ndoa kufanya uchunguzi wa ugonjwa huo, kabla ya kuingia kwenye ndoa ili kujua hali zao na kuanza tiba mapema.
