
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa( TAKUKURU), kudhibiti mianya ya rushwa katika fedha za miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali, ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana.
Ametoa kauli hiyo leo alipotembelea na kukagua ujenzi wa jengo la ofisi za TAKUKURU mkoani Iringa, ambapo amemtaka Mkandarasi kukamilisha ujenzi wa jengo hilo ifikapo mwezi Juni mwaka huu kama ilivyopangwa, ili watumishi wa taasisi hiyo waweze kufanya kazi zao katika mazingira mazuri.
“Tukawe watu wa kupekenyua pekenyua kwenye miradi hii inayotekelezwa na serikali kwani kuna watu wanatumia vibaya fedha za serikali, penyeni huko kuwadhibiti ili miradi ya maendeleo ikamilike kwa wakati na kwa viwango kama ilivyokusudiwa,”. Mhe. Simbachwene
Amefafanua kuwa, TAKUKURU inatakiwa kuhakikisha inasimamia na kudhibiti fedha zisipotee lakini bila kuathiri maendeleo ya miradi ya kimkakati inayotekelezwa nchini.
