Back to top

Takwimu za wenye ulemavu kusaidia utungwaji sera

01 July 2022
Share

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. George Simbachawene amesema upatikanaji wa takwimu sahihi za msingi za Watu Wenye Ulemavu zitawezesha kutungwa kwa sera wakilishi na kusaidia kupima utekelezaji wa malengo mbalimbali ya kitaifa, kikanda na kimataifa.
.
Waziri Simbachawene ameyasema hayo kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa katika kongamano la kuwajengea uelewa watu wenye ulemavu kuhusu Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022. 
.
Mhe. Simbachawene alisema  kwa mujibu wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III) na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG)  yote imeweka mkazo katika kuhakikisha Watu Wenye Ulemavu sio tu wanakuwa sehemu ya mipango ya maendeleo ya nchi bali  wanapewa kila fursa za kujiendeleza katika nyanja zote za maendeleo kama wananchi wengine.
.
Katika kuhakikisha kuwa jamii ya Watu Wenye Ulemavu wanakuwa sehemu ya mchakato mzima wa Sensa ya Watu na Makazi, Serikali imezingatia ushiriki wao katika hatua zote za utekelezaji wa zoezi hili la kitaifa. Ushiriki wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu nchini (SHIVYAWATA) ni ishara ya ujumuishaji huo,” alisema Mhe. Simbachawene.
.
Pia aliitaka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania Bara, na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Tanzania Zanzibar kuendelea kuboresha mbinu za ukusanyaji wa taarifa za hali ya ulemavu nchini, kushirikiana na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na Watu Wenye Ulemavu kwa lengo la kuwatambua na kuwahudumia.
.
Ofisi za takwimu ziendelee kujumuisha maswali yanayolenga kupata taarifa za hali ya ulemavu nchini kwenye tafiti mbalimbali zinazofanywa na Ofisi hizo na Ofisi ya Waziri Mkuu ione  uwezekano wa kuanzisha mfumo wa Kiutawala wa Kukusanya Taarifa za Hali ya Ulemavu Nchini,” alieleza