
Shirika la umeme mkoa wa Arusha limeendelea na msako wa wezi wa umeme wanaohujumu shirika na kufanikiwa kukamata watuhumiwa saba wilayani Arumeru waliojiunganishia nishati hiyo kinyemela bila kujali madhara yanayoweza kujitokeza ikiwemo uharibifu wa miundombinu ya shirika na hata vifo.
Msako huo umefanyika usiku katika maeneo mbalimbali ya mji mdogo wa Ngaramtoni na Ilkiding'a ,zoezi ambalo afisa usalama wa TANESCO mkoani humo Dominick Merey anasema ni endelevu na kwamba watuhumiwa wote watafikishwa kwenye vyombo vya sheria .
Akizungumzia athari za miundombinu ya shirika inayosababishwa na uunganishaji huo holela ,mdhibiti wa mapato wa shirika hilo mhandisi Hassan Lumuli anasema mashine za Transfoma ndizo zinazoathirika zaidi kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watumiaji tofauti na idadi iliyopangwa.
Baadhi ya wakazi wa Arusha wanapongeza uwepo wa zoezi hilo ambalo wanashauri liwe endelevu kuwabaini wahujumu hao ambao wanasema wamekua chanzo kikubwa cha kupungua kwa umeme.