
Shirika la Umeme nchini (TANESCO), limesema hali ya upatikanaji wa Umeme katika baadhi ya maeneo nchini, imekuwa duni kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali, iliyosababisha miundombinu ya umeme, zikiwemo nguzo na transfoma kuanguka.
.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Shirika hilo imebainisha kuwa wataalamu wake katika maeneo mbalimbali nchini, wamekuwa wakifanya juhudi za kufanya marekebisho katika miundombinu iliyopata hitilafu na hata kuharibika kutokana na mvua hizo.
.
Pia Shirika hilo limesema kuwa limekuwa likipata changamoto katika baadhi ya maeneo kwa wataalamu wake kufika kwa haraka na kurekebisha miundombinu iliyoharibika kutokana na baadhi ya miundombinu ya barabara na madaraja kuharibika.
.
Aidha Shirika hilo limewakumbusha wateja wake kuchukua tahadhari kwa kukaa mbali na miundombinu ya umeme hasa katika kipindi hiki cha mvua kwani ni hatari kwa usalama wao na mali zao.
