Back to top

Tanzania ,China kuimarisha mahusiano ya kimkakati.

09 October 2020
Share

Tanzania na China zimekubaliana kuendeleza mahusiano ya kimkakati baina yao ili kuwezesha uwepo wa ulingo sawa miongoni mwa mataifa katika kusimamia maslahi na maendeleo ya nchi husika katika jumuiya za kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi ameyasema hayo jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke na kusisitiza umuhimu wa Mataifa kuheshimiana na kutokubali kuingilia uhuru wa mambo ya ndani ya nchi kwa kisingizio cha haki za binadamu,demokrasia ama jambo lolote jingine.

Ameongeza kuwa mazungumzo hayo ya kimkakati yalilenga pia kutambua kuwa mwaka huu ni mwaka wa 55 tangu Tanzania na China zisaini mkataba wa urafiki ambao uliweka msingi wa mahusiano makubwa na ya dhati  katika nyanja za ulinzi na usalama,afya,kilimo, elimu na miundo mbinu ambapo mpaka sasa China ni Taifa linaloongoza hapa nchini kwa uwekezaji wa moja kwa moja.

Kwa upande wake Balozi wa China hapa Nchini Mhe. Wang Ke amesema China wakati wote ni Rafiki mwaminifu na wa kudumu wa nyakati zote kwa Tanzania na kwamba kutimiza miaka 55 ya urafiki wa nchi hizo ni kielelezo tosha na siku zote wataendelea kuuheshimu na kuuenzi urafiki huo.