
Serikali ya Tanzania imekutana na Umoja wa Ulaya (EU) kujadili masuala mbalimbali yanayohusu Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA) kati ya Umoja huo na Tanzania.
Akiongea wakati wa kikao cha wataalamu kutoka Tanzania na EU kilichofanyika Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara amesema kikao hicho kinalenga kujadili makubaliano yaliyokwama awali kutokana na Tanzania kutokuwa tayari kuridhia baadhi vipengele vilivyomo kwenye mkataba huo.

Prof. Kahyarara amesema Tanzania haikukubaliana na baadhi ya vipengele vya mkabata wa EPA na kuona kuwa ni vigumu kuingia katika makubaliano ya mkataba huo kabla ya kurekebisha vipengele hivyo.
Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Mhe. Manfredo Fanti amesema majadiliano hayo yanalenga kuangalia vipengele vya mkataba ambavyo Tanzania ilionesha mashaka katika kikao kilichopita ili kuvipatia ufumbuzi na kusonga mbele kwa pamoja hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania sasa inatoa kipaumbele katika utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi.
Kikao hicho kinatokana na mazungumzo ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyafanya alipokuwa katika ziara ya kikazi nchini Ubelgiji ambapo alikutana na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya, Bw. Charles Michael mwezi Februari 2022.
