
Waziri waAfya Mhe.Ummy Mwalimu amesema Ili kuweza kuutokomeza ugonjwa wa malaria, kunahitaji rasilimali zaidi na uwajibikaji wenye kuleta matokeo chanya kwenye mapambano dhidi ya malaria.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameeleza hayo Jijini Newyork Marekani, alipokuwa akiwasilisha taarifa ya mapambano dhidi ya Malaria kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Phillip Isdor Mpango, kwenye kikao cha kujadili ufadhili wa mapambano dhidi ya malaria Afrika kupitia Umoja wa Viongozi wa Afrika katika Mapambano dhidi ya Malaria (ALMA).
Waziri Ummy amesema kuwa Tanzania inaendelea kujiimarisha kiuchumi kutokana na athari za janga la UVIKO-19 hivyo ni dhahiri kwamba rasilimali zinahitajika zaidi ili kuweza kufikia malengo ya kupambana na malaria.
Waziri Ummy amesema Tanzania inaendelea kuweka mkazo zaidi kwenye mapambano dhidi ya Malaria kwa kushirikiana na Sekta binafsi, Asasi za kiraia na Jamii kwa ujumla juu ya kukabiliana na ugonjwa wa Malaria.
Pamoja na hayo Waziri Ummy amebainisha kuwa Tanzania hivi karibuni imezindua Baraza la Kutokomeza Malaria ambalo lina jukumu la kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali zaidi, kuelimisha jamii dhidi ya Ugonjwa huo ili kuongeza nguvu zaidi za mapambano dhidi ya Malaria.
