
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii jinsia wazee na watoto Mhe Ummy Mwalimu amesema Tanzania ipo hatarini kukumbwa na ugonjwa wa ebola kutokana na muingiliano wa watu kutoka mataifa ya jirani hususani mikoa ya inayopakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambapo ugonjwa huo umesababisha vifo vya watu 17 katika mji wa Biroko ulioko katika jimbo la Equator nchini Congo.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dodoma Waziri Mhe Ummy amesema mpaka sasa hakuna taarifa za uwepo wa ugonjwa wa Ebola nchini ambapo amesema kutokana na muingiliano wa watu hasa wasafiri kuna kila sababu ya mikoa inayopakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuchukua tahadhari.
Aidha katika hatua nyingine Waziri Mhe Ummy ameitaka jamii kuacha mila potofu kuhusu ugonjwa huo na kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa kwa watoa huduma za afya pale wanapohisi dalili za maambukizi ya ugonjwa huo nchini ambazo ni pamoja na homa kali ya ghafla na maumivu ya misuli.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa kinga kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, jinsia, wazee na watoto Dr Leonard subi amesema mpaka sasa ugonjwa wa ebola hauna kinga na kwamba Tanzania haijawahi kupata ugonjwa huo ingawa nchi jirani zimepata ugonjwa huo.