Back to top

TANZANIA KUIMARISHA UCHUMI, BIASHARA EXPO 2025 OSAKA

27 May 2025
Share

 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Bi. Latifa Khamis, amesema Maonesho ya biashara ya Dunia ya Expo 2025 Osaka, lengo lake kuu ni  kuwaunganisha wafanyabiashara wa pande zote mbili ili kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara.

Bi. Latifa alieleza kuwa TanTrade, ambayo ni chombo kikuu cha kuratibu biashara za kimataifa, iliratibu kongamano hilo kwa kuzingatia sekta za kimkakati ambazo zimeonyesha mafanikio ya kibiashara kati ya Tanzania na Japan, sekta hizo ni pamoja na nishati, madini, kilimo, huduma za kifedha, afya, utalii na uwekezaji. 

Amesema Kupitia kongamano hilo, wafanyabiashara kutoka pande zote wamepata fursa ya kujadiliana namna ya kushirikiana katika kukuza biashara na uwekezaji wa muda mrefu ambapo Bi. Latifa alibainisha kuwa kongamano hilo limezaa matunda makubwa ambapo hati sita za makubaliano (MoUs) zimesainiwa. 

Kongamano hilo lilifunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa na limewaleta pamoja wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania na Japan katika Ukumbi wa Hoteli ya Westin, Osaka, ikiwa ni sehemu ya ushiriki wa Tanzania katika Maonesho ya Dunia ya Expo 2025 Osaka, yanayoendelea hadi Oktoba 13, 2025.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Majaliwa amesisitiza kuwa Serikali ya Tanzania imejipanga kuhakikisha kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 inatekelezwa kwa mafanikio, ikilenga kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa kati wa juu, wenye pato la kati ya USD 4,000 hadi 8,000 kwa mwaka. 

Miongoni mwa makubaliano hayo ni Makubaliano kati ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Umoja wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Japan (AFRECO), unaolenga kushirikiana katika masuala ya elimu na utafiti, wenye thamani ya USD bilioni 1.5 (takriban TZS trilioni 4.03), Makubaliano kati ya Hospitali ya Benjamin Mkapa, Chuo Kikuu cha Dodoma na Tokushukai Medical Group ya Japan, kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha kisasa cha Upandikizaji wa Figo, chenye thamani ya TZS bilioni 28.