Back to top

TANZANIA KUSHIRIKIANA NA CHUO MAPISHI CHA HISPANIA.

28 July 2024
Share

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekubaliana kushirikiana na Chuo cha Mafunzo ya Mapishi cha Basque (Basque Culinary Center) cha nchini Uhispania kilichojikita katika kutoa mafunzo, kufanya tafiti, ubunifu na kufanya uendelezaji wa utalii wa vyakula (Gastronimy Tourism) na lishe. 

Hayo yamebainika katika kikao kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) na Mkurugenzi Mkuu wa Chuo cha Mafunzo cha Basque, Joxe Mari Aizega wakati wa ziara ya kutembelea Kijiji cha Utamaduni cha Umuzi kilichopo jijini Victoria Falls nchini Zimbabwe iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism).

Lengo la kushirikiana na chuo hicho kinachoongoza duniani kwa Sayansi ya Utalii wa Vyakula, Utafiti na Ubunifu ni kukuza Utalii wa Vyakula nchini Tanzania.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Kairuki ameomba mashirikiano na chuo hicho katika utoaji wa elimu ya mapishi, kuwajengea uwezo wapishi wa nchini Tanzania pamoja na wakufunzi wa Chuo cha Taifa cha Utalii, pia kuendeleza tafiti za vyakula, maendeleo ya utalii wa mapishi na namna ya kuboresha vifaa vya mapishi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Mapishi cha Basque, Joxe Mari Aizega amesema taasisi yake iko tayari kushirikiana na nchi zinazotaka kuendeleza Utalii wa Vyakula na pia kuhakikisha ushirikiano kati ya taasisi hiyo na Tanzania unakuwa thabiti na wa muda mrefu.