Back to top

TANZANIA KUWA MFUAJI MKUBWA WA NISHATI

20 September 2023
Share

Waziri Mkuu, Mhe.Kassim Majaliwa amefungua Kongamano la Tano na Maonesho ya Nishati Tanzania na amesema Serikali imedhamiria kuwa mfuaji mkubwa  wa Nishati.

Mhe.Majaliwa ameyasema hayo baada ya kufungua kongamano hilo la siku mbili, linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Amesema Tanzania haitegemei kufua umeme kwa kutumia maji pekee, bali inaendelea kuweka mkazo katika ufuaji wa umeme kwa kutumia nishati nyingine kama gesi na jua.

Waziri Mkuu amesema katika kongamano hilo la kimataifa la Nishati, ambalo limehusisha viongozi na wadau kutoka katika mataifa mbalimbali Duniani litajadili namna bora ya kukabiliana na tatizo la upatikanaji wa Nishati.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko, amesema wameendelea kutekeleza mipango mbalimbali waliojiwekea katika kuhakikisha umeme unapatikana wakati wote nchini.

Dkt.Biteko amesema kampuni zaidi ya 100 za Nishati kutoka katika maeneo mbalimbali duniani zinashiriki katika kongamano hilo ambalo lilitanguliwa na mkutano wa viongozi wa Nishati.