Back to top

TANZANIA NA KENYA KUTATUA VIKWAZO VISIVYO VYA KIUSHURU.

23 March 2024
Share

Tanzania na Kenya zimekubaliana kuendelea kutatua vikwazo vya kibiashara visivyo vya kiushuru kwa kuwa na Mpango wa pamoja wa kuwianisha tozo, ada , ushuru, ada na sheria au taratibu zinazoathiri biashara baina ya pande hizi mbilI masharti mengine yanayoathiri biashara pamoja na kuwezesha ufanyaji biashara mpakani kwa saa 24 ili kukuza biashara baina ya nchi hizo kila siku, kila mwezi na kila mwaka.
 

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato akiwa na Waziri wa  Uwekezaji, Biashara na Viwanda wa Kenya Mhe. Rebbecca Miano baada ya kusaini na kukabidhiana Tamko la Pamoja la Makubaliano ( Communique) wakati wa Mkutano wa nane (8) wa Kamati ya Pamoja ya Biashara baina ya Tanzania na Kenya ngazi ya Mawaziri uliofanyika Kisumu nchini Kenya.
 
Akifafanua zaidi kuhusu makubaliano yaliyotiwa saini , Mhe Byabato amesema  Mkutano huo ulitambua kuwa katika siku 30 zilizopita, baadhi ya vikwazo visivyo vya kiushuru vimeondolea ili kukuza biashara na uchumi baina ya nchi hizo kwa kasi na kuimarisha uhusiano na Kenya ambayo ni Mshirika muhimu wa kibiashara wa Tanzania.
 
Amesema vikwazo hivyo ni pamoja  na kuruhusu kuondolewa kwa zuio la kuingiza chai nchini kutoka Kenya, kuondolewa kwa zuio la kuingiza pombe aina ya Konyagi kwenda nchini Kenya, kuondolewa kwa zuio la kusafirisha mbao kwenda Kenya kupitia mpaka wa Horohoro uliokuwa umezuliwa na Shirika la Viwango nchini Kenya. 

Naye Waziri wa  Uwekezaji, Biashara na Viwanda wa Kenya Mhe. Rebbecca Miano amesema Kenya iko tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuondoa vikwazo vya kibiashara visivyo vya kiushuru ili kukuza biashara na uchumi  pamoja na kuimarisha umoja wa wananchi wa nchi zote mbili.

Aidha amebainisha kuwa Nchi hizo mbili zimekubaliana kushughulikia baadhi ya vikwazo kwa njia za kiutendaji na mamlaka mbalimbali kutoka pande zote mbili na kuimatisha utaratibu wa kufuatilia utekelezaji wa makubaliano na kubadilishana taarifa kuhusu maeneo ya ushirikiano baina ya nchi hizo. 

Mkutano huo wa nane ni utekelezaji wa Maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Dkt. William Samoei Ruto yaliyolenga kuondoa vikwazo vyote vinavyoathiri biashara  ili kuimarisha uhusiano wa biashara. 

Aidha, Mkutano huu wa nane ulilenga kushughulikia vkiwazo vilivyobaki katika Mkutano wa Saba wa Biashara baina ya nchi hizo uliofanyika tarehe 9-12 Machi 2022 huko Zanzibar na unatarajiwa kufanyika Julai 2024 ukilenga kupunguza au kuondoa kabisa  vikwazo vilivyobaki ili kukuza biashara na uchumi wa nchi zotw mbili.