Back to top

Tanzania yaiomba Global Fund kusaidia vifaa tiba.

23 February 2022
Share

Tanzania imeuomba Mfuko wa Dunia (Global Fund) uisaidie Vifaa Tiba ili viende pamoja na juhudi za serikali za kujenga miundombinu ya afya kwa kasi ili kuboresha masuala ya tiba kwa wananchi.

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.Mwigulu Nchemba ametoa ombi hilo Dar es Salaam alipozungumza na Mkuu wa Idara ya Afrika ya taasisi ya Global Fund, Bwana Lienden Morrison aliyeko nchini kwa ziara ya kikazi.

Amesema Rais Samia ameilekeza Wizara ya Fedha na Mipango itafute rasilimali fedha itakayotumika kwa ajili kununua vitendea kazi vitakavyokuwa na hadhi ya majengo ya kisasa yanayojengwa hivi sasa na kuwafanya wananchi wapate huduma bora za afya karibu na maeneo yao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Afrika wa Global Fund Bwana Linden aliipongeza Tanzania kwa kushirikiana na Mfuko wake katika kupiga vita maradhi ya Kifua Kikuu, Malaria na UKIMWI pamoja na namna ilivyokabiliana na ugonjwa wa UVIKO 19 kwa umahiri mkubwa.