
Tanzania imepiga hatua katika utoaji mikopo ya nyumba ambapo jumla ya mikopo 6,182 imetolewa hadi sasa ikilinganishwa na mikopo 579 iliyotolewa kufikia mwaka 2009
Aidha, muda wa urejeshaji mikopo umeongezeka kutoka miaka 15 hadi 25 sambamba na riba ya mkopo kupungua kutoka asilimia 20 - 22 mwaka 2009 hadi asilimia 15-19 zinazotozwa sasa.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula katika Mkutano Mkuu wa 41 wa Taasisi ya Shelter Afrique unaoendelea kwenye Mji wa Victoria Falls nchini Zimbabwe ambapo Tanzania inahudhuria kama mwanachama wa Taasisisi hiyo.
Akichangia mada kuhusu jukumu la Benki Kuu kwenye soko la nyumba katika Bara la Afrika huku akitoa uzoefu wa Taasisi ya ‘Tanzania Mortage Refinance Company’ iliyoanzishwa kufuatia utekelezaji wa mradi wa mikopo ya nyumba uliokuwa ukisimamiwa na Benki Kuu, Dkt Mabula amesema kumekuwa na mafanikio makubwa toka kuanzishwa taasisi hiyo ambapo kwa sasa jumla ya Benki na Taasisi za fedha 33 zinatoa mikopo ya nyumba tofauti na ilivyokuwa kabla ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo ambapo benki 3 tu ndizo zilizokuwa zikitoa mikopo.
