Back to top

TASNIA YA MAZIWA KUNUFAIKA NA PROGRAMU YA BBT MIFUGO

02 June 2023
Share


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega  amesema Wizara yake ipo mbioni kuanzisha programu ya "BBT" kwa upande wa tasnia ya maziwa ambapo tayari ameshaielekeza Bodi ya Maziwa nchini na kurugenzi ya uzalishaji na masoko kutoka Wizarani kwake kushirikiana na washirika wa maendeleo wa sekta ya Mifugo na Taasisi za fedha ili kuanza utekelezaji wa programu hiyo katika mikoa ya Kagera na Mbeya ambako kuna kiasi kikubwa cha  maziwa.

Amesema kuwa Wizara yake ipo tayari kuanzisha programu hiyo katika Mikoa  ya Mbeya na Kagera kwa sababu Mikoa hiyo inazalisha maziwa kwa wingi hivyo anaamini itakuwa rahisi kupata matokeo kwa haraka mara baada ya kuifungamanisha rasilimali hiyo katika mnyororo wa thamani.

Waziri Ulega amebainisha hayo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Unywaji Maziwa Duniani yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Chipukizi mkoani Tabora.

"Nina furaha kutumia jukwaa hili kutangaza jambo hilo ambalo tunaamini mbali na kutatua changamoto ya ajira kwa vijana wetu litaenda kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maziwa kwenye viwanda vyetu nchini," amesema Mhe. Ulega.

Kadhalika amesisitiza kuwa anataka kuona vijana wanapata maeneo katika mashamba yetu ya Serikali na watengenezewe mfumo mzuri wa kuzalisha maziwa wapeleke katika viwanda vyenye uhitaji wa maziwa.