Back to top

"TBA WABANENI WADAIWA WANAOSUASUA"-WAZIRI BASHUNGWA

08 February 2024
Share

Waziri wa Ujenzi, Mhe.Innocent Bashungwa, ameuagiza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuongeza nguvu ya ukusanyaji wa madeni ya kodi ya pango na majengo kwa Wizara, Taasisi na Watumishi waliopanga kwa Wakala huo ambao wamekuwa wakisuasua kulipa kwa wakati.

Ametoa agizo hilo Jijini Dodoma, katika kikao cha uwasilishaji wa madai na madeni ya TBA, ambapo amesisitiza zoezi la awamu ya pili linaloendelea lilete matokeo mazuri zaidi ya ile ya awali ili fedha zinazopatikana zisaidie katika utekelezaji wa miradi mingine.

Bashungwa ameitaka TBA kuhakikisha inayaangalia kwa karibu na kuyaendeleza maeneo yake katika sehemu mbalimbali nchini ili kuepusha migogoro ya ardhi inayojitokeza katika maeneo hayo kutokana na uvamizi.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Eng. Aisha Amour, ameitaka TBA kuweka utaratibu mzuri wa ulipaji wa kodi na kukumbusha madeni mara kwa mara kwa wapangaji wake ili kutolimbikiza madeni hayo na mpangaji kushindwa kulipia kwa wakati.

Akitoa taarifa, Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro, ameeleza kuwa kuanzia mwezi Julai – Disemba, 2023 Wakala huo uliajiri Dalali ambaye alianza kukusanya madeni katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Arusha na Tanga ambapo jumla ya takribani Shilingi Bilioni 21 zilikusanywa.