
Kampuni ya huduma za mawasiliano ya Tigo Tanzania imezindua huduma ya Sako kwa Bako na What’s app, bure yenye lengo la kuwawezesha wateja wao kutumia huduma ya Whatsapp bure mara baada ya kununua kifurushi chochote cha mtandao huo ikiwa ni muendelezo wa kampuni hiyo ya kusherehekea kufikisha wateja zaidi ya milioni 20.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Afisa Mkuu wa biashara wa Tigo Tanzania, Bw. Isack Nchunda, amesema kuwa kampeni hiyo kabambe ya "Sako kwa Bako na WhatsApp bure," inawapa wateja wao sababu mahususi ya kutumia mtandao namba moja Tanzania kwa ubora.
Afisa huyo Mkuu wa Tigo Tanzania aliendelea kwa kusema ''Kampeni hii ni uthibitisho mwingine kuwa Tigo tunadhamiria kufikisha huduma za kidigitali kwa watanzania wote huku tukiendelea kusherehekea hatua muhimu ya kufikisha huduma zetu bora kwa watanzania zaidi ya milioni 20. Tunafarijika sana kuona watanzania wanavyoendelea kutuamini na kuwa sehemu ya familia yetu, hivyo hatuna budi kuendeleza ubunifu ili kukidhi mahitaji yao.''
''Kampeni ya "Sako kwa Bako na WhatsApp bure, ni hatua kubwa na muhimu inayolenga kuleta mapinduzi ya huduma za kidijitali nchini kote hasa wakati huu ambapo tumefanya uwekezaji mkubwa na hatimae kuhakikisha kuwa mtandao wetu wa 4G umeenea kila kona ya Tanzania. Hivyo kwa wateja wetu kunufaika na uwekezaji huu, kila watakaponunua kifurushi chochote kile cha siku, wiki au mwezi wataweza kufurahia huduma ya WhasApp BURE. Kwa ubunifu huu, wateja watapata fursa ya kuwasiliana na ndugu, jamaa na hata kuweza kuboresha shughuli zao za kila siku ikiwemo biashara, masomo, n.k.
Kufuatia uzinduzi wa hivi karibuni wa simujanja inayotumia teknolojia ya 4G ya Energizer U652S, Tigo tunaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuleta suluhisho za kidijitali zenye mchango chanya kwenye safari ya kidigitali ya wateja wetu.
