Back to top

TRA yataka elimu ya mlipakodi iingizwe katika mitaala ya elimu nchini.

20 October 2018
Share

Kamishna  mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania -TRA  Bwana CHARLES KICHERE amesema mamlaka hiyo ipo katika hatua za mwisho kukamilisha taratibu za kuzishirikisha taasisi nyingine za serikali zinazojihusisha na elimu, ili elimu ya ulipaji kodi iingizwe katika mitaala ya elimu nchini.

Amewaambia wanafunzi na walimu wa baadhi ya shule za msingi na sekondari katika mikoa ya Dar es salaam na Pwani kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuifanya elimu ya ulipaji kodi na umuhimu wake uanze kufahamika kwa undani tangu ngazi za chini za elimu.

Naye Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Mlipakodi wa mamlaka hiyo Bwana RICHARD KAYOMBO amesema mamlaka imeweka utaratibu wa kuandaa mashindano yanayohusiana na ufahamu wa ulipaji wa kodi kwa wanafunzi wa shule za Sekondari ili kuwafanya wanafunzi hao wawe chachu kwa jamii kuhusu masuala ya ulipaji wa kodi.

Baadhi ya washiriki wa shindano hilo wamesema limekuwa zuri kwao, kwani wameweza kufahamu umuhimu wa ulipaji kodi na jinsi ambavyo wanaweza kutumia ushawishi wao katika jamii kuhusiana na kuhimiza jamii husika kulipa kodi kama inavyotakiwa.