
Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, amekaribishwa 'kishujaa' katika Kongamano la Kitaifa la Republican, ikiwa ni mara ya kwanza kwa rais huyo wa zamani kuonekana hadharani tangu alipoponea chupuchupu katika jaribio la kuuawa.
Trump aliwasili katika Jukwaa la Fiserv huko Milwaukee, Wisconsin kwenye mapokezi yaliyojaa shangwe siku ya Jumatatu, siku chache baada ya kupigwa risasi sikioni na mtu anayetaka kumuua wakati wa mkutano wa kampeni huko Butler, Pennsylvania.
Wajumbe wa chama cha Republican walisimama na kushangilia wakati Trump akiingia uwanjani, huku akiwa amefungwa bandeji nene kwenye sikio lake la kulia.
Trump, ambaye alionekana kuguswa, hakuhutubia mkutano huo, lakini alitabasamu na kupungia mkono umati huku wafuasi wakiimba “Pigana! Pambana! Pigana”huku wakiwa wamekunja ngumi na kunyanyua juu.