Back to top

TUMEJIPANGA KUONDOKANA NA KILIMO CHA KUJIKIMU-NDAKI

05 August 2022
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Mashimba Ndaki amesema kuwa Serikali imeshaanza kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha sekta ya kilimo inayojumuisha pia mifugo na Uvuvi inabadilika kutoka kwenye hatua ya kujikimu mpaka kuwa kilimo biashara.

Mhe. Ndaki ameyasema hayo wakati wa hotuba yake ya Ufunguzi wa maonesho ya Nanenane kanda ya kati yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma ambapo amebainisha kuwa baada ya Serikali kubaini changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi kama miongoni mwa sababu zilizoshusha ukuaji wa uchumi wa sekta hiyo ilichukua hatua ya kuanza kuboresha miundombinu itakayotumiwa na wakulima, wafugaji na wavuvi hata kwa wakati wote bila kuathiriwa na mabadiliko hayo.

"Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya uchumi ya nchi yetu ya mwaka 2021, ukuaji wa uchumi wa kilimo kwa maana ya kilimo mazao, mifugo na uvuvi ulishuka kutoka asilimia 4.9 mwaka 2020 hadi asilimia 3.9 mwaka 2021 na zipo sababu nyingi zillizopelekea hali hiyo ikiwa ni pamoja na janga la ugonjwa wa uviko 19 lakini kubwa kabisa ni upungufu mkubwa wa mvua ulitokea mwaka 2021 na wakulima, wafugaji na wavuvi wetu kufanya kilimo cha kujikimu ambacho hakitoi mchango wa kutosha kwenye uchumi wao na Taifa kwa ujumla"Amesema Mhe. Ndaki.

Mhe. Ndaki ameongeza kuwa dhamira ya Serikali katika kutekeleza azma hiyo imeanza kuonekana kupitia bajeti za Wizara za Kilimo na ile ya Mifugo na Uvuvi hivyo amewataka  wakulima, wafugaji na wavuvi kuunga mkono jitihada hizo za Serikali ili kuongeza kiwango cha uzalishaji wa mazao yote yatokanayo na kilimo, mifugo na uvuvi na mchango wake kwenye pato la Taifa.

"Na kwa kuwa moja ya maeneo ambayo Serikali imeongeza fedha ya kutosha ni eneo la umwagiliaji, tumeamua kufanya shughuli zetu ziende kwa pamoja  ili kuwafanya wakulima, wafugaji na wavuvi waweze kuongeza tija zaidi ambapo sasa popote patakapojengwa miundombinu ya umwagiliaji, itawekwa na miundombinu ya kunyweshea mifugo na pale tutakapoweka miundombinu ya kunyweshea mifugo itawekwa na miundombinu ya umwagiliaji"Amesisitiza Mhe.Ndaki.

Akielezea namna sekta yake ilivyojipanga kupokea mabadiliko hayo, Kaimu katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya Mifugo Dkt. Charles Mhina amesema kuwa miongoni wa njia ambazo sekta yake huzitumia ili kubadili fikra za wafugaji wakati wa maonesho ya Nanenane  ni kuandaa maonesho ya paredi ya Mifugo ambayo hujumuisha mifugo kutoka kwenye Taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo pamoja na wafugaji binafsi.

"Niwashukuru sana wote mliofika kwenye paredi ya mwaka huu na lengo letu huwa ni kuwafanya wafugaji waachane na ufugaji wa asili na kuingia kwenye ufugaji wa kisasa, nadhani hata nyie mmeona jinsi ng’ombe waliopita mbele yenu walivyo na siha nzuri na mmesikia kiwango chao cha uzito na uzalishaji wa maziwa"Amesema Dkt.Mhina.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia sekta ya Uvuvi Dkt.Rashid Tamatamah amesema kuwa sekta yake imejipanga kuunga mkono juhudi hizo za Serikali za kuhakikisha wanaondokana na uvuaji samaki wa kujikimu kwa kuelekeza nguvu kwenye ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba ambao amebainisha kuwa ndio unaongoza kwa uzalishaji wa samaki wanaofugwa hapa nchini.