
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi, amewataka wafugaji nchini kuongeza mwitikio wa kuchanja mifugo dhidi ya magonjwa mbalimbali ili kuimarisha afya ya mifugo, kuongeza uzalishaji na kupunguza hatari ya maambukizi ya magonjwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
Dkt. Bitanyi ametoa wito huo mjini Morogoro wakati wa kikao cha pamoja kati ya TVLA na timu ya Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP) unaotekelezwa chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Kikao hicho kililenga kujadili maeneo ya ushirikiano katika utekelezaji wa mradi huo.
Amesema bado kuna mwitikio mdogo wa wafugaji wadogo katika kuchanja mifugo yao licha ya uwepo wa chanjo zinazozalishwa na TVLA, huku wafugaji wakubwa wakionesha ushiriki mkubwa zaidi katika kampeni za chanjo.
Amesema moja ya maeneo yanayopaswa kupewa kipaumbele kupitia C-SDTP ni udhibiti wa ugonjwa wa tupa mimba (Brucellosis), ambao ni miongoni mwa magonjwa yanayoathiri mifugo na kupunguza uzalishaji wa maziwa.
Amewasisitiza wananchi kutumia maziwa salama na kuhakikisha wanachemsha maziwa kabla ya kuyatumia ili kujikinga dhidi ya magonjwa yanayoweza kuambukizwa kupitia maziwa yasiyo salama.
Dkt. Bitanyi amesema TVLA ina jukumu la kufanya uchunguzi wa magonjwa ya mifugo, kuzalisha chanjo, kufanya tafiti mbalimbali za kisayansi, kudhibiti ubora wa viuatilifu vya mifugo pamoja na kupima ubora na usalama wa vyakula vya mifugo.
Amesema TVLA pia inaendelea kuimarisha afya ya mifugo kupitia uzalishaji wa chanjo, tafiti na utoaji wa ushauri wa kitaalamu kwa wafugaji ili kuongeza tija katika sekta ya mifugo.
Ameongeza kuwa TVLA huzalisha aina saba za chanjo za mifugo zinazotumika nchini, ambapo chanjo moja ni ya kuku na nyingine ni za wanyama kama ng’ombe, mbuzi na wanyama wengine.
Kwa mujibu wa Dkt. Bitanyi, kulinda afya ya mifugo ni hatua muhimu katika kulinda afya ya binadamu kwa kuwa takwimu za dunia zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya magonjwa yanayowapata binadamu yanatokana na wanyama.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kitaifa wa C-SDTP, Lazaro Kapela, amesema mradi huo unatekelezwa katika mikoa minane na halmashauri 21 za Tanzania Bara pamoja na mikoa mitano ya Zanzibar.

Amesema mradi huo wa kimkakati unalenga kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafugaji, zikiwemo upatikanaji wa mbegu bora za ng’ombe kupitia teknolojia ya uhimilishaji, upatikanaji wa malisho bora, huduma za afya ya mifugo pamoja na miundombinu ya maji.
“Bila malisho bora na maji ya kutosha, ng’ombe hawezi kuwa na afya nzuri wala kuzalisha maziwa ya kutosha. Kupitia mradi huu tunafanya uwekezaji katika visima, mabwawa ya maji na mifumo ya kuboresha uzalishaji wa malisho ili kuongeza tija kwa wafugaji,” amesema Kapela.
Ameongeza kuwa mradi huo pia unashirikiana na TVLA katika kuimarisha afya ya mifugo kupitia matumizi ya chanjo na huduma za kitaalamu zinazolenga kuongeza uzalishaji wa maziwa na kupunguza hasara zinazotokana na magonjwa.
Kapela amesema mradi huo utawekeza pia katika vituo vya kukusanyia maziwa ili kuwaunganisha wafugaji na masoko na kuwahakikishia soko la uhakika la mazao yao.
“Vituo vya kukusanyia maziwa vitakuwa kiunganishi muhimu kati ya mfugaji na soko. Lengo ni kuhakikisha mfugaji apate soko la uhakika na thamani stahiki ya bidhaa zake,” amesema.
Amebainisha kuwa mradi huo wa miaka 10 ulianza mwaka 2024 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2034 kwa gharama ya dola za Marekani milioni 231.
Naye Afisa Mwandamizi wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Mradi huo, Goodluck Masawe, amesema mradi unatarajiwa kunufaisha kaya 140,000 sawa na watu zaidi ya 700,000.
Amesema kati ya wanufaika hao, asilimia 40 ni wanawake, asilimia 30 ni vijana na asilimia tatu ni watu wenye ulemavu watakaofikiwa moja kwa moja na huduma za mradi huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Benezeth Lutenga Malinda, amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa inayotekelezwa na wizara hiyo kwa lengo la kuongeza uzalishaji, ubora na usalama wa mazao ya mifugo kwa masoko ya ndani na nje ya nchi.
Amesema wizara imeweka msisitizo katika kuimarisha mifumo ya afya ya mifugo, maabara na ufuatiliaji wa magonjwa ili kuhakikisha maziwa na bidhaa nyingine za mifugo zinazozalishwa nchini zinakuwa salama kwa matumizi ya binadamu.
“Mradi huu umejipanga kuimarisha mifumo ya maabara, ufuatiliaji wa afya ya mifugo na kuhakikisha mifugo inayozalishwa na kusambazwa inakidhi viwango vya ubora na usalama. Tunataka kuona maziwa yanayozalishwa nchini yanakuwa na ubora unaotakiwa na yanakuwa salama kwa mlaji,” amesema Dkt. Malinda.
Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya wizara, taasisi zake na wadau wa sekta ya mifugo wa Tanzania Bara na Zanzibar utakuwa msingi muhimu wa kufanikisha malengo ya mradi huo.
“Tunatarajia mradi huu kuongeza uzalishaji wa maziwa, kuimarisha usalama wa chakula na kuboresha lishe ya Watanzania pamoja na kuongeza kipato cha wafugaji kupitia mifumo bora ya uzalishaji na masoko,” amesema.
