
Wizara ya Afya kupitia mpango wa Taifa wa kutokemeza ugonjwa wa vikope(Trakoma)imewataka wakuu wa mikoa katika Halmashauri 38 zilizoathiriwa na ugonjwa huo zikiwemo, Wilaya nne za mkoa wa Manyara zenye wagonjwa 2,442 kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa na kuepusha maambukizi ya vikope kwa watoto wenye umri chini ya miaka 10 ambao wapo katika hatari ya upofu.
Meneja mpango wa Taifa kitengo cha udhibiti magonjwa matano yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kupitia wizara yenye dhamana, Dokta.George Kabona ametoa agizo hilo wilayani Babati wakati wa uzinduzi wa utokomezaji wa ugonjwa huo, ambapo serikali imetenga shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kampeni hiyo.
Akizindua kampeni ya nyumba kwa nyumba kwa Wilaya 4 za Kiteto, Simanjiro, Mbulu na Babati zilizoathiriwa, Mkuu wa mkoa wa Manyara, Bw.Makongoro Nyerere amesema utalenga kutibu lakini pia kudhibiti watoto ili wasimabukizwe.
Takribani wagonjwa 13,000 nchini wanakabiliwa na madhara ya macho baada ya kupata maambukizi ya vimelea vinavyosababisha ugonjwa wa vikope.
