
Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson ametolea ufafanuzi juu ya uhalali au uharamu wa kuwepo kwa wabunge 19 wa viti maalum wa CHADEMA bungeni na kusema kuwa uharamu haupo na hawawezi kuwa haramu na wakawepo bungeni.
"Uharamu haupo, kwa sababu hawezi kuwa haramu halafu akawa mle ndani (bungeni), lakini nataka nifafanue jambo moja, nchi yetu inaendeshwa kidemokrasia lakini kisheria, jambo moja tu ambalo linasubiriwa, labda tu niseme, ni watu kumaliza michakato yao inayohusika...".Dk.Tulia Ackson-Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ameeleza kwamba kuna masharti ya mbunge kuwa ndani ya bunge, na moja wapo ni awe amedhaminiwa na chama, hivyo wabunge hao wangekuwa hawana chama wasingekuwa bungeni.
"Huko nyuma mabunge yaliyopita wameshawahi kuondolewa wabunge kwa sababu katiba yetu inataka mbunge lazima awe mwananchama wa chama fulani, kwa hiyo mtu akifukuzwa uanachama na chama fulani, anakuwa hana uhalali wa kuwepo bungeni, lakini sababu ya demokrasia ile michakato lazima iwe imemalizwa, bunge liletewe taarifa mahususi kwamba mtu huyu sio mwanachama wa chama fulani, anaondoka".Dk.Tulia Ackson-Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
