Back to top

Uhamiaji Kigoma walalamikiwa kuwabambikizia kesi za uraia wananchi.

08 June 2021
Share

Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma ujiji mkoani Kigoma wamelalamikia vitendo vya baadhi ya maafisa wa idara ya uhamiaji mkoani Kigoma kufanya vitendo vya uonevu kwa kuwakamata na kuwabambikia makosa ya uraia wananchi ambao ni raia halali wa Tanzania huku wakiwaacha watu wasio raia ambao wamekuwa wakiishi bila kuzingatia sheria.
.
Madiwani hao wamesema maafisa wa idara ya uhamiaji wamekuwa wakiwakamata watanzania na kuwalundika pamoja bila kuzingatia misingi ya utu pamoja na kuwashusha abiria kwenye mabasi bila kutenda haki licha ya kuwa raia, huku wakiwaacha wahamiaji ambao wanaishi na kufanya shughuli zisizo halali katika maeneo ya kumbi za starehe na maeneo mengine ya kibiashara.
.
Akitoa ufafanuzi kuhusu sintofahamu hiyo Afisa kutoka idara ya uhamiaji mkoa wa Kigoma, Dominic Kibuga, amesema idara hiyo imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi kuhusu kusumbuliwa na maafisa wa idara hiyo, na kwamba hatua zimekuwa zikichukuliwa pamoja na kuhakikisha hakuna usumbufu unaojitokeza katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya usafiri.