Back to top

Ukosefu wa maji wasababisha watu kuliwa na Mamba mto Malagarasi.

24 August 2019
Share

Wananchi wa kijiji cha Malagarasi katika wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma wamemweleza Naibu waziri wa Maji Mhe.Jumaa Aweso kusikitishwa na kitendo cha serikali kupitisha miundombinu ya miradi ya maji katika kijiji hicho kuelekea maeneo mengine wakati wao wakiendelea kupata adha ya ukosefu wa maji hali inayosababisha baadhi yao kupoteza maisha kwa kuliwa na mamba waliopo mto Malagarasi.

Wakizungumza mbele ya Naibu waziri wa Maji Mhe.Jumaa Aweso wamesema wamekuwa wakiwajibika kulinda na kutunza vyanzo vya maji katika mto Malagarasi na wanashangazwa na hatua ya serikali kutumia vyanzo hivyo kupeleka maji maeneo mengine huku wao wakiendelea kuteseka kwa kukosa maji kwa miaka mingi pamoja na hofu ya kukamatwa na Mamba.

Naibu Waziri wa maji Jumaa Aweso ambaye yupo katika ziara ya kukagua miradi ya maji mkoani Kigoma amesema maelekezo ya serikali ni kuhakikisha wananchi wote wanapata maji kwa kuanzia na wale wanaoishi jirani na vyanzo vya maji na sio vinginevyo.

Katika hatua nyingine Mhe.Aweso amewataka wananchi wa kata ya Nguruka kuwa wavumilivu wakati serikali ikifanya jitihada za kupeleka umeme katika kijiji hicho utakaosaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa katika kijiji cha Nguruka.