Back to top

Ulega aagiza ziundwe kamati za usuluhishi migogoro .

14 September 2021
Share

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amewataka viongozi wa  Serikali kuanzia ngazi za Vitongoji, Vijiji, Kata na Wilaya kuhakikisha wanaunda kamati za maridhiano kwa ajili ya kusuluhisha migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo imekuwa ikijitokeza katika baadhi ya maeneo na kuleta madhara kwa jamii.

Ulega ametoa agizo hilo kwenye ziara aliyoifanya katika Kijiji cha Nakiu Kilichopo Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi baada ya kupokea kero zilizohusu migogoro mingi iliyoanza kujitokeza katika Wilaya hiyo inayowahusisha wakulima na wafugaji.

Katika Mkutano huo wananchi wa Kijiji hicho walililalamikia Jeshi la  Polisi katika Wilaya hiyo kwa  kutochukua hatua za haraka pale wanapopelekewa taarifa za wafugaji wanaolisha mifugo yao katika mashamba ya wakulima.

Wakulima hao wamesema kuwa wafugaji wanaofanya vitendo hivyo wengi ni wahamiaji katika maeneo hayo na hivyo wamekuwa wakiwasababishia matatizo makubwa ikiwemo kuharibiwa kwa mazao yao na wanapotaka kufanya jitihada za kulinda mazao yao wanaishia kupata kipigo.

Kufuatia malalamiko hayo yaliyotolewa na sehemu kubwa ya wakulima hao, Waziri Ulega ametoa maelekezo kwa Watendaji wa Serikali kuanzia ngazi za chini kuanzisha kamati za usuluhishi ili ziwe zinashughulika na migogoro hiyo mapema kabla haijakuwa mikubwa na kuleta madhara.

Ulega ameongeza pia kwa kulitaka Jeshi la Polisi wilayani humo kuhakikisha wanatenda haki kwa kila mtu na kwa usawa ili kuondoka lawama zinazowakabili za kuonekana wanawapendelea wafugaji kuliko wakulima.

Aidha, Waziri Ulega ametumia ziara hiyo kukemea vitendo vya kujichukulia Sheria mkononi vinavyofanywa na wakulima pamoja na wafugaji akisema kuwa kufanya hivyo ni kosa na ni miongoni mwa vitendo vinavyochangia uvunjifu wa amani.