Back to top

ULEGA AHIMIZA UWEKEZAJI SEKTA ZA MIFUGO, UVUVI NA KILIMO

19 May 2023
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Abdallah Ulega, amewahimiza Mawaziri Wenzake wa nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)  wanaosimamia Kilimo, Chakula, Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji kushirikiana na Sekta Binafsi kuongeza uwekezaji katika sekta za Mifugo, Uvuvi na Kilimo ili kuimarisha Usalama wa Chakula na kukuza uchumi wa Nchi hizo.

Waziri Ulega ametoa rai hiyo wakati akitoa neno la utangulizi katika Mkutano wa 16 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaosimamia Kilimo, Chakula, Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji uliofanyika mkoani Dar es Salaam.

Amesema uwekezaji ukiongezeka utachechemua uzalishaji na hivyo kuimarisha Usalama wa Chakula na pia kutashamirisha biashara ya chakula miongoni mwa nchi hizo na kukuza uchumi wao.

Ameongeza kuwa kwa upande wa Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kufanya uwekezaji kwenye sekta za mifugo na uvuvi na kilimo ziweze kuongeza uzalishaji ili ziwe na mchango mkubwa zaidi katika pato la Taifa.

Miongoni mwa hatua alizozitaja ambazo Dkt.Samia Suluhu Hassan amezichukua ni pamoja na kuwawezesha vijana mitaji ya kujiajiri kupitia sekta za mifugo, uvuvi na kilimo, kuwawezesha maafisa ugani ili watoe huduma sahihi na kwa urahisi kwa wananchi, Kutekeleza Mpango Kabambe wa sekta ya Uvuvi wa Mwaka 2021/2022- 2036/2037 na kufanya kampeni kubwa ya uchanjaji na uogeshaji wa mifugo nchini.

Mkutano huo ulikutanisha Mawaziri 7 kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Sudani Kusini, Jamhuri ya Kongo (DRC) na Burundi.