Back to top

ULEGA AHIMIZA ZAO LA DAGAA KWENDA KIMATAIFA.

20 May 2022
Share

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Abdallah Ulega amekutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la Kusafirisha Mizigo (DHL) nchini Tanzania, Bi.Fatma Abubakar kujadiliana namna Serikali na shirika hilo watakavyoweza kushirikiana kufungua zaidi masoko ya Kimataifa ya zao la Dagaa na Mwani.

Akizungumza katika majadiliano yao hayo, Waziri Ulega amesema zao la dagaa kwa muda mrefu limekuwa likiuzwa katika nchi mbalimbali za Afrika, Ulaya na Amerika lakini biashara hiyo imekuwa ikifanywa kienyeji sana jambo ambalo limesababisha nchi na watu wake kutokuona tija kubwa ya zao hilo.

"Pamoja na dagaa kuuzwa katika masoko ya nje bado watu wanafanya kienyeji sana, tunatakiwa tuwekeze katika kuliongezea thamani zao la dagaa na kulifungasha vizuri ili liweze kuthaminika katika masoko ya kimataifa na litanunuliwa kwa wingi kuliko ilivyo hivi sasa"Amesema Ulega.

Ameongeza kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na dagaa kwa wingi kuanzia baharini na katika maji baridi isipokuwa bado halijawekewa mnyororo wa thamani mzuri ili kulipa heshima yake na kuweza kuwainua wananchi.

"Tuweke mipango mizuri ya masoko ya dagaa na mwani ili kusudi tuweze kuona namna tunavyoweza kushirikiana katika kuyaboresha mazao hayo na kuyatafutia masoko ya uhakika nje ya nchi"Amefafanua.

Amesisitiza kuwa ni muhimu sasa zao la dagaa likapata hadhi yake, mnyororo wa thamani wa zao hilo uimarishwe ili Wafanyabiashara waondokane na uuzaji wa dagaa katika magunia na waanze  kuwaweka katika vifungashio vizuri vitakavyovutia biashara ya kimataifa.

Aidha ameongeza kuwa ni muhimu kuanza kuelimisha  Vikundi vya Ushirika vya uvuvi ambavyo tayari vipo kwani kwa  kufanya hivyo itakuwa rahisi kuwafikia Wafanyabiashara hao  na kuwaelekeza namna ya  kuboresha biashara zao ili ziweze kukidhi masoko ya kimataifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la Kusafirisha Mizigo (DHL), Bi.Fatma Abubakar alisema kuwa walianza kuwawezesha Wafanyabiashara wa dagaa katika ukanda wa Ziwa Tanganyika lakini wanakusudia kuupeleka mradi huo pia mkoani Mwanza ili Wafanyabiashara mkoani humo waweze kujua namna ya kufanya ili waweze kuuza dagaa wao nje ya nchi. 

"Kwa upande wetu sisi tunapenda tufanye kazi pamoja  ili tuweze kuwasaidia wafanyabiashara wetu wa Tanzania na waweze kujikimu kimaisha"Amesema Abubakar

Kuhusu zao la Mwani, Abubakar alisema kwa sasa wameanzisha mradi wa kuwawezesha wakulima wa mwani waliopo Visiwani Zanzibar na  wanategemea kuendelea kuwaelimisha ili zao hilo liweze kuwafaidisha zaidi.

Sehemu ya timu ya maafisa kutoka Shirika la Kimataifa la kusafirisha mizigo ( DHL) wakifuatilia mazungumzo baina ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega na Mkurugenzi Mtendaji wa DHL Tanzania, Bi. Fatma Abubakar (hawapo pichani) katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma