Back to top

ULEGA AKABIDHI MICHANGO KWA WAATHIRIKA WA MAFURIKO HANANG.

11 December 2023
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amefika Wilayani Hanang, Mkoani Manyara kutoa pole na kukabidhi michango ya wadau na Wizara kwa wananchi walioathirika na mafuriko wilayani humo.

 Mhe. Ulega alisema Wizara yake imepokea kwa masikitiko makubwa  tukio la mafuriko hayo yaliyotokea na kusababisha kupoteza maisha ya Watanzania pamoja na uharibifu wa mali na mifugo.

Amesema Wizara yake kwa kushirikiana na wadau katika sekta ya mifugo na uvuvi wakiwemo  ASAS, Bajuta International,  Dalberg International, Karie Kinana, APOKA, TAFMA, TABROFA na TPBA) kwa pamoja wameandaa vitu mbalimbali na kuvikabidhi kwa Kamati ya Maafa ya Kitaifa kwa ajili ya uratibu wa namna nzuri ya kuvifikisha kwa familia na walengwa wote.

Miongoni mwa vitu ambavyo amevikabidhi ni pamoja na Ng’ombe 13, Mbuzi 20, Trei 90 za mayai, Fedha tasilimu jumla ya shilingi Milioni 5, Maziwa katoni 300, Sembe, Maharage na Chumvi.

Aidha, alibainisha kuwa Wizara yake itaendelea kushirikiana na Kamati ya Taifa ya Maafa na Uongozi wa Mkoa na Wilaya ili kubaini uharibifu wote wa miundombinu ya mifugo na kuirejesha katika hali yake kwa haraka ili kuhakikisha mifugo inaendelea kupata huduma stahiki na kuwezesha wafugaji kunufaika na mifugo yao kwa maendeleo ya nchi.

Waziri Ulega aliendelea kusisitiza kuwa Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kusimama na watanzania wote katika hali zote ambazo zinawapata watanzania akiongeza kuwa wao kama wasaidizi wake wapo imara kuhakikisha adhma yake ya kuendelea kuwaletea maendeleo Watanzania inatimia.

Waziri Ulega amekabidhi vifaa hivyo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama kwa niaba ya waathirika wa mafuriko hayo.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga ametoa shukrani zake za dhati kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Wadau mbalimbali wanaoendelea kujitokeza kuwafariji katika kipindi hiki kigumu.