Back to top

Ulega ampa maagizo DC Komba kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji.

22 September 2021
Share

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Hashim Komba kuhakikisha anawapanga wakulima na wafugaji katika maeneo waliyopangiwa ili kuondosha migogoro inayoikabili Wilaya hiyo.

Ametoa kauli hiyo wakati akiongea na wakulima na wafugaji wa Kata za Matekwe, Kilimarondo, Kiegei na Mbondo katika Wilaya hiyo ya Nachingwea, Mkoani Lindi kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili.

Ameeleza kuwa ili Wilaya hiyo iondokane na migogoro ya Wakulima na Wafugaji ni lazima Serikali isimamie mpango wa matumizi bora ya ardhi ambao tayari wanao.

"Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya mfugaji au mkulima anayefanya shughuli katika eneo ambalo hakupangiwa mtoe mpeleke katika eneo analopaswa kufanya shughuli zake, ni lazima tusimamie utaratibu tuliojiwekea kwa mujibu wa sheria,"amesema Ulega

Kuhusu tatizo la maji ya kunyweshea mifugo linalowasumbua Wafugaji wa maeneo hayo, Ulega alisema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ametenga Shilingi Milioni 480 kwa ajili ya kujenga Bwawa la kunyweshea Mifugo litakalojengwa katika Kijiji cha Matekwe Kilichopo Wilayani humo ili Wafugaji wawe na maji ya uhakika  wakati wa kiangazi.

"Sio bwawa tu, Rais Mama Samia atawajenge Josho kwa ajili ya kuogeshea mifugo, Milioni 18 zitatolewa kwa ajili ya kazi hiyo, Sasa nitashangaa sana nikiona wafugaji mnaendelea kuzagaa," Ulega

Aidha, alitumia fursa hiyo pia kuwaonya Wakulima  na Wafugaji hao kuacha vitendo vya kujichukulia Sheria mkononi kwani havifai na vinahatarisha amani katika jamii.

Naye Mkuu wa Wilaya wa Nachingwea, Hashim Komba alimuhakikishia Naibu Waziri Ulega kuwa maelekezo yote aliyoyatoa atayafanyia kazi na kisimamia sheria ili utaratibu ufuatwe.