Back to top

ULEGA AWAALIKA WAWEKEZAJI BBT MIFUGO

13 June 2023
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Misri kuja kushirikiana na Serikali katika  kuwawezesha vijana na wafugaji wengine kufuga kisasa na kunenepesha mifugo kupitia programu ya BBT Mifugo.

Hayo yamefahamika wakati wa ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega na ujumbe kutoka nchini Misri waliyoifanya katika Ranchi ya Kongwa iliyopo Wilayani Kongwa, Jijini Dodoma kwenda kuona namna wanavyoweza kushirikiana katika  kuwawezesha vijana na wafugaji wengine kufuga kisasa na kunenepesha mifugo kupitia programu ya BBT Mifugo.

Amesema lengo la Wizara ni kufanya ushirikiano na Wawekezaji hao  kuingia mikataba na vijana ya kuwawezesha kuzalisha mifugo bora ambayo itawafanya  wawekezaji hao  kuwa na uhakika wa kupata nyama bora kwa ajili ya kuuza nchini Misri.

Hivyo, Mhe. Waziri amewashauri wawekezaji hao kuona uwezekano wa kuwawezesha rasilimali fedha vijana kwa njia ya mikataba ili wazalishe mifugo bora ambayo itakuwa chanzo cha  uhakika cha wawekezaji hao kupata nyama bora lakini vilevile itawasaidia  vijana hao kuwa na uhakika wa ajira kupitia programu hiyo ya  BBT mifugo.

Aidha, Mhe. Ulega amesisitiza kuwa kama wawekezaji hao watakuwa tayari kuwezesha vijana kupitia BBT mifugo yeye yuko tayari kuielekeza Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kushirikiana nao katika kutekeleza programu hiyo katika Ranchi ya Kongwa.