Back to top

ULEGA: TUNATAKA MAZIWA YAKUZE AJIRA NCHINI.

24 June 2022
Share

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Abdallah Ulega amesema Serikali imejipanga kuhakikisha kunakuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji katika tasnia ya maziwa ili iweze kutoa fursa nyingi za ajira kwa vijana na kina mama hapa nchini.

Ulega ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kukagua viwanda vya kuchakata maziwa vilivyopo Jijini Dodoma.

Amesema kuwa msimamo wa Serikali ni kuona uwekezaji katika tasnia ya maziwa unashamiri ili zao hilo liweze kuongezewa thamani na kwa kufanya hivyo wananchi wengi wataweza kujipatia kipato kupitia mnyororo wa thamani.

"Tumepeleka mapendekezo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuondoa kodi nyingi ambazo zikiondoka zinakwenda kunawirisha tasnia ya maziwa, kwa mfano kodi zinazohusu vifungashio ili wawekezaji waweze kuzalisha kwa gharama nafuu na kukuza ajira kwa jamii"Amesema.

Halikadhalika, ameongeza kuwa Serikali imedhamiria kukutana na wadau wa tasnia ya maziwa nchini kujadili nini kifanyike ili maziwa mengi yanayozalishwa na wafugaji yaenda viwandani kwa ajili ya kuchakatwa na kuongezewa thamani ili ajira nyingi ziweze kupatikana kwa vijana na kina mama.

"Mpaka hii leo maziwa mengi bado yanauzwa kienyeji huko mitaani jambo ambalo linasababisha upotevu mkubwa wa maziwa, kw mfano ni asilimia 3 tu ya maziwa yote yanayozalishwa na wafugaji ndio yanaenda viwandani, na ndio maana Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inafanya jitihada kubwa kuondoa vikwazo vya kikodi ili mzalishaji wa Kiwandani awe na uwezo wa kununua kwa bei nzuri kwa yule mfugaji ili wafugaji washawishike kupelekea maziwa yao viwandani"Amefafanua.

Aidha, amesema kuwa Serikali inakwenda kuweka vituo vya kukusanyia maziwa sehemu mbalimbali nchini, na mwaka huu Serikali imetenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kazi hiyo kwa kushirikiana na wadau ili maziwa mengi yaweze kukusanywa na kuingia viwandani.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe.Jabir Shekimweri amesema kuwa katika jitihada za kuwezesha wafugaji kuinuka kiuchumi mkoani humo, kupitia mfuko wa kusaidia vijana, watu wenye ulemavu na wanawake wametoa mikopo kwa vikundi 12 ili wafanye ufugaji wa kisasa na kuzalisha maziwa mengi zaidi. 

Ameongeza kwa kusema kuwa Serikali ya mkoa ipo bega kwa bega na wawekezaji ili lengo la uwekezaji na ufugaji wenye tija waweze kuufikia kwenye makao ya nchi.