Back to top

Umilikishaji ardhi kuondoa changamoto kwa wanawake.

15 May 2022
Share

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Ridhiwani Kikwete amesema faida kubwa na kipaumbele katika zoezi la kupanga, kupima na kumilikisha ardhi ni kupambana na ukatili dhidi ya wanawake ikiwemo kuondoa changamoto ya akina mama kukosa nguvu ya kumiliki ardhi haki aliyoieleza kuwa itapatikana kwa kutoa hati ya pamoja kati ya mume na mke.

Naibu Waziri Kikwete amesema hayo wakati akihutubia wananchi wa Mbalizi halmashauri ya wilaya ya Mbeya wakati wa uzinduzi wa mradi wa kupanga, kupima na kumilikishwa ardhi unaosimamiwa na Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) na baadae kushiriki zoezi la ugawaji hati kwa wananchi waliokamilisha taratibu za kumilikishwa ardhi.

Aidha, ameongeza kuwa kupima ardhi kutawezesha kutatua migogoro isiyo ya lazima kwa kuwa kazi hiyo inahusisha upimaji shirikishi ambao baada ya wataalamu kujiridhisha wakati wa zoezi hilo hati hutolewa bila ya kuwepo migogoro yoyote.

‘’Kumekuwepo na spidi ndogo ya wananchi kwenda kuchukua hati zao lakini niwambie ninyi kuna wakati utafika mutahitaji kulima kadiri ya taratibu za serikali na kuepuka uharibifu wa mazingira kuna wakati itabidi zitumike mbinu za kitaalam ili kuendelea na kilimo.’’Ameongeza Ridhiwani Kikwete Naibu Waziri Wizara ya Ardhi.

Naibu Waziri Ridhiwani alizitaja faida za kuwa na hati kuwa ni pamoja na kuthaminiwa na kupatiwa uhakika wa kupata huduma za kibenki kwa mmiliki, kuongeza thamani ya ardhi tofauti na ile ardhi isiyopimwa aliyoieleza kuwa haina thamani yoyote hapa nchini.