Back to top

UNESCO:Corona inaweza kuwa chanzo cha watoto wengi kutorudi shule.

23 June 2020
Share

Ripoti mpya ya hali ya elimu duniani ya shirika la Umoja wa Mataifa, UNESCO imesema karibu watoto milioni 258 hawakwenda shule mnamo mwaka 2018. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 17 ya vijana ulimwenguni kote.

Ripoti hiyo pia imeeleza kwamba mamilioni ya wavulana na wasichana wanabaguliwa katika mifumo ya elimu kwa sababu ya asili zao au ulemavu walionao. 

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay amesema janga la corona limeathiri zaidi shughuli za elimu na kwamba tatizo hilo la kiafya linaweza kuwa chanzo cha kuwafanya watoto wengi wasirudi shuleni hasa wasichana kutoka familia masikini.

UNESCO imesema kwenye ripoti yake kwamba kwa bahati mbaya, makundi yenye matatizo mbalimbali yanawekwa au yanasukumwa nje ya mifumo ya elimu kupitia maamuzi ambayo yanasababisha kutengwa  kimitaala, malengo yasiyofaa katika ufundishaji, vitabu vinavyotumiwa, ubaguzi katika ugawaji wa rasilimali, vurugu na hata kupuuzwa kwa mahitaji ya wanafunzi.

UNESCO inazihimiza nchi kuzingatia watoto walio kwenye mazingira magumu wakati shule zitakapofunguliwa tena baada ya kufungwa kwa sababu ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.