Wananchi wanaojishughulisha na uvuvi katika ukanda wa Ziwa Tanganyika, wameunga mkono hatua ya serikali ya upumzishwaji wa shughuli za uvuvi katika ziwa Tanganyika, ili kulipa nafasi ziwa kuongeza kiwango chake cha uzalishaji wa samaki.
Wananchi hao wameunga mkono hatua hiyo wakati wa hafla ya kukabidhi vizimba vya kufugia samaki, boti za kisasa za uvuvi na doria na pia kupata elimu na uelewa kuhusu upumzishaji wa shughuli za Uvuvi Ziwa Tanganyika iliyofanyika katika Mwalo wa Katonga, mkoani Kigoma.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wawakilishi wa wananchi, akiwemo Mbunge wa Kigoma Mjini, Mhe. Kilumbe Ng’enda amesema kuwa muda ambao umepangwa ziwa kupumzishwa ni muafaka kwa sababu kipindi hicho ni maarufu kwa jina la ‘kilimia’ ambapo ziwa huwa linajifunga lenyewe na kufanya kupungua kwa Mazao ya samaki.
Naye, Mbunge wa Kigoma Kusini, Mhe. Nashon Bidyanguze alisema kuwa mwanzoni walikuwa wanapinga kufungwa kwa ziwa kwa sababu wananchi walikuwa hawana elimu ya kufungwa kwa ziwa lakini sasa hawawezi kuendelea kupinga kwa sababu tayari serikali imepeleka boti na vizimba kwa ajili ya wananchi kutumia kufuga samaki katika kipindi ambacho ziwa litakuwa limefungwa.
Wakati akikabidhi boti na vizimba kwa wanufaika wanaofanya shughuli zao katika Ziwa Tanganyika, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa Boti na Vizimba hivyo ili wananchi watumie kufugia samaki kama njia mbadala ya kujipatia kipato katika kipindi ambacho ziwa litakuwa limepumzishwa.
Aidha, Waziri Ulega amewataka wanufaika wa boti hizo na wengine wote wanaoendesha shughuli za Uvuvi Ziwa Tanganyika na Nyasa kutumia zana hizo kwa malengo yaliyokusudiwa, huku akiwaelekeza maafisa uvuvi wa ukanda wa Ziwa Tanganyika kutotumia kipindi hicho kuwasumbua wavuvi hususani wavuvi wadogo badala yake waendelee kuwaelimisha.
Katika hafla hiyo, Waziri Ulega amekabidhi vizimba 29 kwa vikundi sita na watu binafsi 16 na Boti 6 kwa ajili ya uvuvi na doria katika mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa.