
Usitishaji mapigano uliokubaliwa katika Ukanda wa Gaza bado haujaanza na shirika la habari la Palestina (WAFA) limeripoti juu ya makumi ya watu waliouawa katika mashambulizi ya Israeli.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Bw.Riyad Al Maliki, amesema watu 52 kati ya waliouawa katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia, Kaskazini mwa Gaza walikuwa wa familia moja.
Wakati huo huo, kumekuwa na ucheleweshaji kwa makubaliano kati ya Hamas na Israel, ambayo yanalenga kuafikia makubaliano ya kusitishwa kwa mapigano kwa muda na baadhi ya mateka kuachiliwa.
Sasa imefahamika kutoka chanzo cha serikali ya Israeli kwamba Hamas, imetoa madai ya ziada kwa mpango huo, ingawa haijulikani wazi madai hayo.
Kama sehemu ya makubaliano hayo, mateka 50 wa Israel wanatarajiwa kuachiliwa huru na Hamas na wafungwa 150 wa Kipalestinawaachiliwe na Israel pamoja na kusimamishwa kwa mapigano kwa muda kwa siku nne.
Awali mpango huo ulikuwa ufanyike Jana lakini ulicheleweshwa hadi leo Ijumaa kufuatia tangazo la serikali ya Israel jana usiku.
