
Utalii wa mazao ya nyuki ikiwemo kunusa mizinga pamoja na kung’atwa na nyuki, umeanza kufanyika mkoani Songwe, katika msitu mkubwa wa asili wa Longisote uliopo Kata ya Hasamba, wilayani Mbozi mkoani humo, unaosifika kuwa na nyuki wenye sumu adimu, ambayo inadaiwa kuwa na faida nyingi kwa binadamu, ikiwemo kuimarisha kinga ya mwili pamoja na mifumo ya upumuaji.
Baadhi ya wadau wa utalii, waliofika katika msitu huo nakufanya utalii wa kunusa mizinga na kung’atwa na nyuki, wanasema zao hilo kwao ni kitu kipya, hivyo ipo haja ya kulitangaza na kuwanufaisha wengi.
Akizungumzia utalii huo Mhifadhi na Afisa Utalii Bw. Probi Kimario, ambaye ni msimamizi wa shughuli hiyo iliyo chini ya mradi wa ufugaji nyuki, unaojulikana kwa jina la 'Mbozi Asali Asilia' anasema kando na kuzalisha asali wameamua kugeukia zao hilo kwa lengo la kukuza sekta hiyo.
Mhifadhi Kimario ameongeza kuwa katika mradi huo, wamekuwa wakitoa mafunzo ya ufugaji nyuki kwa njia ya kisasa kwa makundi mbalimbali ikiwemo aina ya mazao hayo,huku akiomba jamii kujenga utamaduni wa kutembelea maeneo ya utalii yenye vivutio kama hivyo.
