Back to top

VIASHIRIA VYOTE VYA UVUNJIFU WA AMANI VIDHIBITIWE

21 September 2022
Share


Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa, amewataka watendaji wote Serikalini kuweka mkakati wa kudhibiti viashiria vyote vya uvunjifu wa amani katika maeneo yao.
 
Mhe.Majaliwa amesema lengo la agizo ni kusisitiza utekelezwaji wa maono na dhamira ya Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha nchi inaendelea kuwa katika hali ya utulivu ili kuendelea kufikisha maendeleo katika kila eneo.
 
Amesema hayo leo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani yayofanyika katika ukumbi ya Kuringe, Moshi Kilimanjaro.
 
Pia, amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan itaendelea kuchukua hatua na tahadhari zote zinazohitajika ili kuendelea kudumisha amani nchini.
 
Ameongeza kuwa kila palipo na amani, shughuli za kiuchumi na kijamii hufanyika kwa ufanisi mkubwa na hivyo kuchochea maendeleo ya nchi na ustawi wa wananchi kwa ujumla. “Niwasihi wananchi kuendelea kutunza na kuilinda tunu ya amani tuliyojaliwa hapa nchini”
 
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuendelea kuunga mkono ajenda mbalimbali za maendeleo nchini ili kuhakikisha umaskini haugawanyi jamii bali uwe chachu ya kutafuta njia bora ya kujinasua katika hali hiyo.
 
Naye, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa Nchini Tanzania, Zlatan Milisic ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kuwa kinara katika kudumisha amani katika nchi za Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla.
 
Aidha, alitoa wito kwa jamii yote nchini kuacha kuchukulia mzaha suala la uwepo wa amani kwani yapo mahusiano ya karibu kati ya amani na maendeleo.  “Jamii yenye amani inaweza kuweka mipango yake ya maendeleo vizuri na kuitekeleza kwa ajili ya shughuli za maendeleo”
 
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu amesema kuwa viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro wataendelea kusimamia utunzaji wa amani tuliyonayo kwani ni tunu muhimu tuliyojaliwa nchini.
 
“Sisi viongozi wa mkoa wa Kilimanjaro tutaendelea kushirikiana na taasisi zote zikiwemo za dini kwani uwepo wa amani ni msingi wa ustawi wa wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro na Tanzania kwa ujumla”.