
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Wilbroad Mutafungwa, amesema wamekamata vifaa vya ujenzi vilivyoibwa katika mradi wa ujenzi wa Daraja la Dkt.John Pombe Magufuli la Kigongo-Busisi ,ambapo amebainisha kuwa Disemba 08, 2022, Saa 07:30 asubuhi, Jeshi hilo lilipokea taarifa kutoka kwa kampuni ya ujenzi wa daraja hilo ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), kuwa kuna wizi wa vifaa vya ujenzi.
.
Kupitia taarifa za kiintelijensia Jeshi hilo lilifika katika kitongoji cha Busisi madukani ,kwenye nyumba inayomilikiwa na Makona Samwel na kufanya upekuzi kwenye chumba cha Halfani Seif Yusuph, ambaye ni mfanyakazi wa kampuni ya CCECC kama fundi nondo na kukuta vifaa vyote vilivyoibiwa katika mradi huo.
Vitu hivyo, ni pamoja na Mashine Saba za kuchomelea, Stick za kuchomelea vyuma aina ya THJ 422 Box 30, Welding Cable na Drilling Bit mbili ambapo bado kufahamika thamani yake.
.
Uchunguzi wa awali umeonesha mtuhumiwa huyo alishirikiana na Hamfrey William ambaye ni mfanyakazi pia wa kampuni ya CCECC kama fundi wa kuchomelea na mlinzi wa kampuni ya ulinzi COPS SECURITY TANZANIA LIMITED aitwaye Bwire Manyama ambapo mtuhumiwa mmoja ambaye ni Bwire Msiba Manyama (30), Mlinzi wa Kampuni ya COPS amekamatwa kwaajili ya upelelezi zaidi.
