Jeshi la Polisi kupitia Bohari kuu limesema limeendelea kusimamia uzalishaji wa sare za maafisa na askari wa Jeshi la Polisi nchini, Pamoja na kufunga mifumo ya TEHAMA na vifaa vya kisasa vya ushoni Bohari kuu ya Jeshi la Polisi.
Akitoa taarifa hiyo leo Boharia Mkuu wa Jeshi la Polisi Kamishna msaidizi wa Polisi ACP Moses Mziray, amesema Pamoja na kufanyika maboresho makubwa ndani ya Jeshi hilo Bohari kuu pia imepata vifaa vya kisasa vitakavyowezesha kuongeza uzalishaji wa sare za Jeshi hilo huku akimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassani kwa namna ambavyo anawezesha kiwanda hicho kufanya uzalishaji Mkubwa.
ACP Mziray ameongeza kuwa kikosi hicho kimeendelea kushona sare za Jeshi hilo kwa kasi kubwa ili kuondoa upungufu wa sare ambapo amebainisha kuwa mashine za kisasa zilizopo zimeongeza ufanisi mkubwa wa utendaji wa kazi kiwandani hapo huku akimshukuru Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Camillus Wambura kwa namna ambavyo ameendelea kukiangalia kwa karibu na kukiwesesha kiwanda cha Jeshi hilo.
Naye Mkuu wa kiwanda cha ushonaji Bohari kuu ya Jeshi la Polisi Mkaguzi msaidizi wa Polisi A/INSP Jenitha Mtayoba amesema wanaendelea na ushonaji kwa kasi kubwa kutokana na vifaa vya kisasa vilivyopo kiwandani hapo.