Back to top

Vigodoro vyasababisha kushuka kwa ufaulu Malinyi.

05 February 2019
Share

Viongozi wa ngazi mbalimbali wakiwemo madiwani katika halmashauri ya wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro wamekiri sherehe za kukesha maarufu kama vigodoro hasa wakati wa mavuno ya mpunga imechangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi na kuzua tabia hatarishi  miongoni mwa makundi ya vijana kutokana na baadhi yao kutoroka na kwenda maeneo hayo usiku wa manane.

Baadhi ya viongozi wakiwemo madiwani wamekiri ngoma hizo za vigodoro kushamiri zaidi Malinyi msimu wa mavuno ya mpunga, jambo linalofanya tabia za vijana wengi hasa wanafunzi kuharibika na wengine kutoroka masomo.

Mkuu wa wilaya ya Malinyi Majura Kasika naye amekiri kuwa vigodoro ni tatizo  walilobaini limechangia kushuka kiwango cha ufaulu kwa kidato cha nne kutoka asilimia 77 mwaka jana kufikia asilimia 68 na tayari wameweka maazimio kulidhibiti kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya ambapo sasa watakaofanya vigodoro hadi saa 5 usiku kwa siku za kawaida watalipia shilingi 20,000, saa 6 usiku siku za mapumziko na watakaokesha zaidi ya muda huo watalipia shilingi laki.