Vijana wametakiwa kuwasilisha malalamiko yao kuhusu huduma za fedha katika mamlaka husika, ili kupata suluhu haraka pamoja na kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta ya Fedha ikiwemo utapeli, udanganyifu na mikopo yenye riba kubwa maarufu kama mikopo umiza au kausha damu.
Wito huo umetolewa Ikungi mkoani Singida, na Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha nchini kutoka Wizara ya Fedha, Bi. Dionesia Mjema, baada ya kutoa elimu ya fedha katika Kongamano la Vijana wa Wilaya hiyo.
Bi. Mjema alisema Serikali imeweka kanuni na miongozo ili malalamiko hayo yaweze kusikilizwa na kufanyiwa kazi kwa mujibu wa Sheria za Fedha.
“Waende Benki Kuu kama malalamiko yao yanahusu masuala ya benki, kama yanahusu masuala ya dhamana ya masoko na mitaji basi waende Mamlaka ya Dhamana ya Masoko na Mitaji, kama yanahusu bima yapelekwe Mamlaka ya Usimamizi wa Bima na yale yote yanahusiana na mafao ya uzeeni waende Ofisi ya Waziri Mkuu”, alifafanua Bi. Mjema.
Naye Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Bw. Peter Musa alisema wameona ni vema kuialika Wizara ya Fedha kutoa elimu ya Fedha kwa kuwa kwa sasa masuala ya fedha yamekuwa changamoto hususan kwa vijana.
Alisema pamoja na kuwa Wizara imekuwa ikifanya juhudi kubwa za kusambaza elimu hiyo nchini lakini waliona mkusanyiko wa Jukwaa la Vijana katika shughuli za Mwenge ni sehemu muafaka kwa ajili ya kutoa elimu hiyo.
Kwa upande wa vijana walioshiri Kongamano hilo, wameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa elimu hiyo muhimu kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.