Back to top

Vijana wanaongoza kwa magonjwa ya akili nchini.

10 October 2018
Share

Vijana wenye umri kati ya miaka 14 mpaka 25 wanaongoza kwa magonjwa ya akili nchini kutokana na mitindo ya maisha, matumizi ya dawa za kulevya na ulevi wa pombe kupindukia huku idadi kubwa wakishindwa kupata matibabu ya hospitali mapema kutokana na jamii kuhusisha maradhi hayo na imani za kishirikina. 
 
Tanzania inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya afya ya akili ambapo akitoa tamko la Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mganga mkuu wa serikali Profesa Mohamed Kambi anasema nusu ya wagonjwa wote wa akili wako katika umri huo na hawapati nafasi ya kupatiwa matibabu kwa wakati muafaka .
 
Akizungumzia chimbuko la maradhi hayo daktari bingwa wa magonjwa ya akili kutoka taasisi ya magonjwa ya akili Mirembe Dk Damas Andrea anasema hurithiwa kutokana na historia ya familia au ukoo huku akikanusha uvumi kuwa katika watanzania wanne mmoja ana matatizo ya afya ya akili .
 
Kwa upande wake Dk Enock Changalawe anasema matatizo ya afya ya akili kwa asilimia kubwa huwakumba wanaume kuliko wanawake huku asilimia 60 hufikishwa hosipitalini wakiwa wamechelewa baada ya kuanzia kwa waganga wa kienyeji .
 
Siku hiyo kwa mwaka huu kidunia imebeba kauli mbiu isemayo vijana na afya ya akili katika ulimwegu wa mabadiliko.