
Jumla ya vijiji 75 vilivyokuwa na migogoro ya matumizi ya ardhi katika mkoa wa Arusha vimenufaika na hisani ya Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kwake kubaki maeneo yake kufuatia vijiji hivyo kuingia kwenye migogoro ya matumizi ya ardhi na maeneo ya hifadhi.
Mkoa wa Arusha unahusisha vijiji na mitaa 116 kati ya 975 vyenye migogoro ya matumizi ya ardhi na hifadhi, mashamba, ranchi, mapori ya akiba na vyanzo vya maji ambapo taarifa yenye mapendekezo ya utatuzi wake iliwasilishwa serikalini tarehe 23 Septemba 2019 na kutolewa uamuzi na Baraza la Mawaziri.
Katika taarifa hiyo ilipendekezwa vijiji 920 kati ya 975 vyenye migogoro ya matumizi ya ardhi nchini kubaki ingawa baadhi yake vitahusisha marekebisho ya mipaka kwa njia shirikishi na baadhi yake migogoro yake ilishatatuliwa.
"Vijiji na mitaa 116 Arusha kuachiwa vijiji 75 kubaki kwenye maeneo yake ni hisani ya kipekee na tunatakiwa tuiheshimu na tusiitumie vinginevyo kwa sanababu Mhe.Rais Samia alikuwa na uwezo wa kutaka kuviondoa lakini ameridhia maeneo 75 kubaki"Amesema Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula.
Akizungumza na uongozi wa mkoa wa Arusha wakati wa ziara ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta mkoani humo, Dkt.Mabula amesema sambamba na uamuzi wa serikali, uongozi wa mkoa utakuwa na jukumu la kusimamia mpango wa matumizi ya ardhi sambamba kudhibiti vyanzo na vichocheo vyote vya kuzalisha migogoro.

