Back to top

VIJIJI VITUMIE MRADI WA LTIP KUANZISHA HIFADHI

25 March 2024
Share

Vijiji vilivyopangiwa mipango ya Matumizi ya Ardhi kupitia mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) vimetakiwa kuutumia mradi huo kuanzisha hifadhi za vijiji ili kutunza na kuhifadhi misitu, Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa mkoa wa Lindi.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Geophrey Pinda, ambapo amesema vijana wanaweza kutumia hifadhi hizo za misitu zilizobainishwa na mradi wa uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi kwa kuanzisha miradi kama vile ufugaji nyuki na kusema mradi huo unaweza kuwapa faida kubwa kiuchumi. 

Wilaya ya Kilwa ni miongoni mwa Wilaya 15 zilizoongezwa kunufaika na mradi wa LTIP kwa kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji 69 kati ya Vijiji 90 vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa na kufanya Vijiji vilivyofikiwa na mradi huo kuwa 1667 nchi nzima.

Ameongeza kuwa Wizara ya Ardhi kupitia mradi wa LTIP awali ulichagua Wilaya 7 za kutekeleza mradi ambazo ni Maswa, Mufindi, Tanganyika, Mbinga, Chamwoni, Longido na Songwe uliolenga kuboresha usalama wa milki za ardhi kwa kupanga ardhi katika Vijiji 250, kupima na kusajili hati za Hakimiliki za kimila 500,000.

Amesema "Namna nzuri ya kutunza mazingira kwenye maeneo yetu ni kuanzisha miradi inayoweza kusaidia kutunza mazingira na misitu kwa kuanzisha WMA katika vijiji vyenu"Mhe.Pinda

"Misitu yote iliyotengwa kupitia mradi wa LTIP makundi ya vijana yahamasishwe ili yaweze kufuga nyuki sisi kule kwetu tunafuga nyuki na lita moja ya asali tuko mbali kweli kweli" amesema Mhe.Pinda

Mmoja wa waratibu wa mradi wa LTIP wilaya ya Kilwa ambaye ni Afisa Mipango wa Miji wa Wizara ya Ardhi Elisha Mengele alieleza kuwa, mradi wa uboreshaji usalama wa Milki za Ardhi mbali na mambo mengine umelenga  kuwa na maeneo ya hifadhi endelevu, kuondoa migogoro ya mipaka na uwezeshaji vyeti vya ardhi vya vijiji ili kuwa na nguvu ya kisheria kusimamia ardhi yao.

Amesema, kupitia mipango ya Matumizi ya ardhi kwenye halmashauri wilaya ya Kilwa maeneo mbalimbali yametengwa kama vile kupanga maeneo yatakayoendana na uhalisia sambamba na kuhakikisha misitu na maeneo muhimu kuhifadhiwa yanakuwepo.

Kwa upande wao, wananchi wa Kilwa wameonesha kuridhishwa na mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi nchini kwa kuwa umewashirikisha na kutenga maeneo mbalimbali kama vile mifugo, wakulima, misitu ya asili, vyanzo vya maji pamoja na makaburi.

Wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji mradi huo walioueleza kuwa umempa haki kila mtu alipo.