Rais wa Jamhuri ya Muungano Mh. Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi katika nchi za Afrika kuwekeza katika nguvu kazi kubwa ya vijana na wanawake kwa kuwapa elimu, sayansi na teknolojia zitakazowawezesha kutumia rasilimiali zilizopo ili Afrika iwe na mchango mkubwa katika soko la dunia.
Akifungua kongamano la wanawake na vijana katika eneo huru la biashara Afrika jijini Dar es Salaam Rais Samia amesema wanawake na vijana ni jeshi kubwa linaloweza kuharakisha mapinduzi ya kiuchumi afrika likiwezeshwa kutumia fursa hiyo ipasavyo.
Amesema vijana na wanawake wanahitaji elimu, sayansi , teknolojia, mitaji na mikopo ya riba nafuu pamoja na mazingira wezeshi ya miundombinu , masoko na sera zitakazoondoa vikwazo baina ya nchi na nchi katika ukanda wa kibiashara na katika eneo huru la biashara Afrika.
Aidha Rais Samia amesisitiza umuhimu wa kuwa na takwimu sahihi za uzalishaji, usafirishaji na mauzo ya bidhaa katika Bara la Afrika ili kujua wapi kuna soko na bidhaa zipi na wapi zinapatikana kwa wingi ili kufanikisha itifaki nzima ya eneo huru la biashara Afrika.
Amesema upande wa Tanzania unachukua hatua kadhaa zikiwemo za kuweka mazingira wezeshi na kuondoa pengo la kijinsia katika biashara pamoja na vikwazo katika biashara za ukanda wa kiuchumi wa jumuiya ambazo ni mwanachama.
