
Viongozi wa Dini wa Mkoa wa Kagera wameungana kwa pamoja kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Viongozi wa Kitaifa na Serikali kwa kuendelea kudumisha amani, utulivu, upendano na Maelewano.
Ibada hiyo iliyowakutanisha viongozi wa Dini ya Kikristo na Kiislamu imefanyika katika Kanisa Anglikana Mt. Yohana Kimbugu - Muleba, mkoani Kagera.
Akiongoza Ibada hiyo, Askofu wa Dayosisi ya Lweru Kanisa la Anglikana Tanzania, Godfrey Mbelwa amesema viongozi wa Dini na Waumini wana wajibu wa kuwaombea viongozi wa Kitaifa kwani wanafanya kazi kubwa ya kuwaletea wananchi Maendeleo.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa ambaye amemwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewashukuru viongozi wa Dini kwa kuandaa maombi ya kumuombea Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan yaliyoambatana na Harambee ya Ujenzi ya wa Kanisa Parishi ya Kimbugu, Muleba mkoani Kagera.
Katika Harambee ya Ujenzi wa Kanisa, Waziri Bashungwa amewasilisha mchango wa Viongozi wa Serikali, jumla ya Shilingi Milioni 30 na kuahidi kuendelea kushirikiana na viongozi wa Kanisa hilo ili ujenzi ukamilike kwa wakati.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatma Mwassa amewaomba viongozi wa Dini kuendelea kuwasihi waumini kuwa wacha Mungu ili kuwa na hofu ya kutenda maovu kwenye jamii ikiwemo mauaji na ukatili wa kijinsia.