Back to top

Viongozi wa Dini Rukwa kupunguza muda wa ibada kujihadhari na Corona.

31 March 2020
Share

Viongozi wa madhehebu ya dini mkoani Rukwa wamekubaliana kuwa kila dhehebu kulingana na imani zao kuona namna ya kupunguza muda wa kufanya ibada katika misikiti na makanisa mbalimbali ili kukabiliana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19).

Wamekubaliana hayo wakati wa kikao kifupi kilichoitishwa na Mkuu wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Julieth Binyura katika kikao hicho kilicholenga kuwaelimisha viongozi hao juu ya Chanzo, usambaaji na namna ya kujikinga na ugonjwa huo ambao unaendelea kuisumbua dunia huku jukumu la kutoa elimu likifanywa na Mganga mkuu wa mkoa wa Rukwa.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu wakati akieleza namna ya kujikinga na ugonjwa huo alitoa msisitizo kwa viongozi hao kutumia maji tiririka pamoja na sabuni ya maji wakati wa kunawa huku akieleza madhara ya kutumia sabuni ya unga na ya kipande kuwa na tabia ya kushikwa na kila mtumiaji.