Back to top

Vita dhidi ya ukatili kwa wanawake kuimarishwa

13 May 2022
Share

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu amesema Serikali itaendelea kuongeza jitihada katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo pamoja na wizara husika ili kuhakikisha makundi hayo yanakuwa salama.
.
Dkt.Jingu ametoa kauli hiyo wakati akiongoza kikao cha Kamati Elekezi ya Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kilichofanyika Jijini Dodoma kikihudhuriwa na Makatibu Wakuu, wawakilishi kutoka Wizara mbalimbali na wadau wa maendeleo nchini.
.
Katibu Mkuu huyo alisema ipo haja ya kuongeza nguvu katika mapambano hayo kila mdau kwa nafasi yake ili kuongeza jitihada za utekelezaji wa mpango huo kutokana na kuongezeka kwa vitendo na matukio ya ukatili katika maeneo mbalimbali.

“Inabidi tuongeze nguvu yaani Serikali, Wizara za kisekta , Idara,Taasisi, Asasi za kiraia,wadau  na vyombo vya ulinzi katika mapambano haya wote kwa nafasi zetu ili kuongeza kazi ya utekelezaji wa mpango huu na kufikia hilo lazima tuwe na rasilimali kulinda na kutetea makundi ambayo yamekuwa yakiathirika kutokana na vitendo hivyo,”alisema Dkt. Jingu.